NAFASI YA AKILI NA FAHAMU ZA KAWAIDA KATIKA KUNENA KWA LUGHA.

Akili ya binadamu (kwa Kiingereza “mind”]) ni kipawa kinachowezesha kufikiri, kuelewa, kuwasiliana, kujifunza, kupanga na kutatua matatizo. Ni ufahamu uliomo katika ubongo hasa wa binadamu, unaomwezesha hata kutofautisha jambo kwa wema na ubaya wake upande wa maadili na hatimaye kumuongoza katika kufanya maamuzi kwa kutumia hiari yake. (Wikipedia)

Akili ya mwanadamu ni sehemu ya nafsi ya mwanadamu. Na mungu alipomuumba Mwanadamu alimuumba katika utatu. Mwanadamu ni Roho, yenye nafsi na anayeishi katika mwili, hivyo Roho, nafsi na mwili vikatengeneza utatu wa mwanadamu.

Kazi ya mwili ni kukupa kibali na kukuwezesha mwanadamu kuishi katika nnchi (dunia) na ndio maana mwili wa mwanadamu ni mavumbi ya ardhi.

Kazi ya Roho ya mwanadamu ni kiungo kati ya mwanadamu mwenyewe na Mungu, na ndio maana biblia inasema katika Yoh 4:24 kuwa;

“Mungu ni Roho nao wamuabuduo yeye imewapasa kumuabudu katika Roho na kweli.”

Kwa hiyo katika utatu wa mwanadamu, kinachotakiwa na chenye uwezo wa kuwasiliana na Mungu ni Roho na sio nafsi wala mwili.

Nafsi kwa upande mwingine ni kiunganishi kati ya Roho ya mwanadamu na mwili wa mwanadamu, na nafsi haikuumbwa wala haikufanywa bali ilitokea wakati Roho na mwili vilioounganishwa (Mwanzo 2:7). Ndani ya nafsi imo akili, maarifa utashi na hisia. Hivi vyote viko kwenye nafsi na sio katika Roho wala mwili.

Kazi ya nafsi ni kumsaidia mwanadamu kuhusiana vyema na mazingira yake na kufanya maamuzi ya maisha yake. Pamoja na uwezo na umakini mkubwa wa nafsi (akili zikiwamo ndani yake) bado nafsi haina uwezo wa kuhusiana na Mungu kwa mambo ya Rohoni kwa ufasaha. Mambo haya ya kiRoho yanajumuisha maombi na ibada. Ibada inayofanyika katika nafsi huwa na ukomo na ndio maana ni kusudio la Mungu ni sisi tumuabudu yeye katika Roho na kweli.

Kwa habari ya uhusiano wa kunena kwa lugha na akili, biblia inasema katika 1Kor 14: 2

“Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika Roho yake.”

Lakini pia hebu tusome maandiko haya yafuatayo;

1Kor 2 :14

“Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya Rohoni.”

Halafu 1kor 2 13 anasema;

“Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.”

Hebu tusome na mstari huu tena 1 Wakorintho 14:14

“Maana nikiomba kwa lugha, Roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.”

Hebu rudia kusoma tena hiyo mistari hapa chini;

“Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika Roho yake.”(1Kor 14: 2)

“Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya Rohoni.”(1Kor 2 :14)

“Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.”(1kor 2:13)

“Maana nikiomba kwa lugha, Roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.” 1 Wakorintho 14:14

Maandiko haya yanatuonyesha kwa uchache mambo  yafuatayo;

  • Mungu anawasiliana na Roho ya mwanadamu
  • Mwanadamu kwa asili hawezi kupokea mambo ya Roho kwa sababu;
    • hawezi kuyafahamu
    • Kwake huyo ni upuuzi
    • Kwa sababu yanatambulikana kwa jinsi ya Roho.
  • Mambo ya Rohoni yanafundishwa na Roho na ili kuyaelewa lazima utumie maneno ya Rohoni.
  • Njia moja wapo ya kuyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni ni kunena kwa lugha au kuomba kwa Roho kwa sababu unaponena kwa lugha unaongea na Mungu mambo ya siri katika Roho yako.
  • Ukinena kwa lugha akili zako hazina matunda. Biblia ya kiingereza ya amplified inaendelea kueleza (kwa sababu haielewi Roho yangu inachokiomba.)

Kama tulivyoona hapo juu, nafasi ya akili, ufahamu, ujuzi na maarifa ya kibinadamu ni ndogo sana linapokuja swala la kunena kwa lugha, kwa sababu kunena kwa lugha ni jambo la KiRoho na KiMungu na wala sio jambo la kibidanamu wala la uweza wa kibinadamu.

Ninaamini kwamba hadi sasa utakuwa umeelewa ni kwa nini ukinena kwa lugha huwa huelewi maana ya maneno unayoyasema. Kwa hiyo nikutie moyo kwamba unaponena kwa lugha na akili yako isipoelewa unachokinena basi hapo ndio haswaa unanena inavyopaswa.

Ni vizuri kabla hatujamaliza kipengele hiki nikuambie mambo mawili ambayo yatasaidia uelewa wako wa kunena kwa lugha.

Jambo la Kwanza:

Japokuwa unaponena kwa lugha akili zako hazina matunda lakini ni ukweli kwamba unanena kwa lugha kwa kutumia utashi wako na sio kwa kulazimishwa na Roho Mtakatifu.

Hapa ninamaanisha, japo Roho Mtakatifu ndiye anayekupa cha kunena lakini utashi wa kunena au kutokunena uko kwako na sio kwa Roho Mtakatifu. kwa maneno mengine Roho Mtakatifu hawezi kukulazimisha kunena japo anaweza kukushawishi (inspire) kunena katika mazingira fulani fulani.

Mtu haneni kwa lugha pale tu anapokuwa amezidiwa na upako. Unaweza kunena na inatakiwa uweze kunena wakati wowote unapotaka, na utakapotaka kufanya hivyo Roho Mtakatifu yuko tayari kila wakati kukuwezesha kunena kwa lugha.Hivyo basi tunaweza kusema kuwa unaponena akili zako hazina matunda,lakini utashi wa kunena huko unafanyika na akili yako, na uwezo wako wa kunena utaongezeka pale utakapokuwa radhi kumpa Roho Mtakatifu nafasi mara nyingi kadiri inavyowezekana.

Jambo la Pili :

Mungu anaweza kukufunulia katika akili zako na ufahamu wako wa kawaida uweze kufahamu yale ambayo unayanena kwa lugha usiyoifahamu.

Jambo hili linawezekana kwa Mungu kuachilia karama nyingine. Karama hiyo inaitwa karama ya kufasiri Lugha. Kadiri Roho Mtakatifu atakavyoona inafaa anaweza kuachilia karama hii juu yako wewe mwenyewe mzungumzaji wa lugha au akaiachilia kwa mtu mwingine ambaye ataweza kufasiri kile unachokinena kwa siri katika Roho yako.

Mara nyingi hili linatokea kama Mungu anataka huo ujumbe ulifikilie kanisa au uwe dhahiri katika ufahamu wako ili uchukue hatua fulani kuhusiana na hilo. Tutajifunza vizuri karama hii huko mbele.

Mungu akubariki sana, Tafadhali tuonane katika somo linalofuata.

Unaweza pia kumshirikisha ndugu, jamaa au rafiki kwa kubonyeza alama ya mtandao wa kijamii unaoutumia hapa chini.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *