Kama umesoma vizuri sehemu zilizopita hapo juu, utakuwa umekwisha jionea mambo matano ya msingi katika kunena kwa lugha, ambayo ni;
- Kunena kwa lugha kunatendwa na Mtu anayemuamini Yesu (aliyeokoka).
- Kunena kwa Lugha kunafanyika kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
- Lugha inayozungumzwa yaweza kuwa lugha inayozungumzwa hapa duniani.
- Mtendaji (Mnenaji) hapaswi kuwa na ufahamu wala ujuzi wa lugha anayoiongea.
- Kunena kwa Lugha huambatana na muamini kujazwa Roho Mtakatifu/kubatizwa na Roho Mtakatifu.
Hivyo basi ukiyachunguza mambo hayo matano ya msingi utagundua mambo yaliyoko upande wako kuyafanya ni mambo makubwa mawili ambayo yote yanafanyika kwa imani. Mambo hayo ni;
- Kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yako.
- Kujazwa na Roho Mtakatifu.
1.Kumpokea Yesu kama bwana na mwokozi wa maisha yako.
Tumeshajifunza hapo awali ya kwamba kunena kwa lugha ni moja ya ishara za watu wanaomuamini Yesu. Na kwamba Yesu mwenyewe katika kitabu cha Marko 16:17-18 anasema;
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Hivyo basi anayenena kwa lugha ni lazima awe muamini na si vinginevyo.
Na kama basi wewe bado hujaokoka na unataka kufaidi zawadi hii ya Mungu kwa wanadamu, unaweza kuifaidi kwanza kwa kuokoka ambapo biblia katika kitabu cha Warumi 10:9-10 inasema;
” 9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”
Hivyo basi kama unaamini kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu na uko tayari kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu ni Bwana sema sala hii kwa sauti na utakuwa umeokoka na utafaidi yote yanayosemwa katika kitabu hiki kwa maana ya Kunena kwa Lugha na faida ziambatanazo na Kunena kwa Lugha.
Sema maneno haya kwa sauti;
“Eee Bwana Yesu, ninatubu dhambi zangu, karibu moyoni mwangu, uwe Bwana na Mwokozi wa Maisha yangu. Amen”.
Hongera sana kwa kusema sala hii, kama umesema ukiwa unaamini kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu,basi wewe umekwisha okoka.
Kwa kusema maneno hayo huku ukiwa unaamini moyoni, umekwisha kuokoka, unamaisha mapya ndani yako na wewe ni mwana wa Mungu kuanzia sasa (Kwa ufahamu zaidi unaweza kusoma kitabu changu kingine cha Nini Kinatokea unapookoka)
2. Kujazwa na Roho Mtakatifu.
Kama ambavyo tunaokoka kwa imani, vivyo hivyo tunajazwa Roho Mtakatifu kwa imani. ukisoma kitabu cha wagalatia 3:2-7 Utajifunza kuwa kumpokea Roho Mtakatifu ni jambo la imani sawa sawa na kuokoka kulivyo jambo la imani, hebu tosome kwa pamoja;
“2 Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
3 Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?
4 Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.
5 Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
6 Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.
7 Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. “
Kama hivyo ndivyo, basi ni imani yako tu ndiyo inayohitajika ili kujazwa na Roho Mtakatifu, Na imani yenyewe ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na ni bayana ya mambo yasioonekana(Ebr 11:1).
Tunaamini Mungu wetu anasikia maombi na kila tuombalo sawasawa na mapenzi yake analijibu. Yesu mwenyewe anasema katika Luka 11-13;
“10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao? “
Huu ni uthibitisho wa Yesu Mwenyewe kwamba tukimuomba Baba Roho Mtakatifu, hakika atatupa, kwani yeye ni muaminifu sana kuliko wababa wa dunia hii walio waovu lakini wajuao kuwapa watoto wao vipawa na zawadi njema.
Ndugu yangu, imani ni kuwa na hakika na Mambo yatarajiwayo na ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Katika hatua hii kama unamtarajia Roho Mtaatifu kuja juu yako na kukubatiza basi kuwa na hakika kuwa hilo linawezekana pale tunapomuomba baba yetu wa Mbinguni katika jina la mwana wake mpendwa Yesu Kristo.
Mimi mwenyewe nimeshuhudia wengi wakijazwa Roho Mtakatifu pale tulipoomba, hebu kwa imani fuatisha sala hii ukiwa mahali pa utulivu na ukiwa na taraja nawe utampokea Roho Mtakatifu, Sema sala hii kwa sauti ukisema;
“Eee Baba yangu wa mbinguni, naja mbele yako saa hii, nakushukuru kwa sababu umetimiza ahadi yako ya kumwaga Roho wako Mtakatifu kwa wote wenye mwili, ahsante kwa sababu kama vile ulivyoniokoa kwa imani, hivyo hivyo unanijaza Roho wako Mtakatifu siku hii ya leo. Baba ninakushukuru kwa Roho wako Mtakatifu, ninaomba sasa Baba unibatize kwa Roho wako Mtakatifu, katika jina la Yesu nimeomba na kupokea, amen. “
Kwa sala hii amini ya kuwa umebatizwa na Roho Mtakatifu na kwamba umepokea uwezo wa kunena kwa lugha.endelea kuomba maombi ya kumsukuru Mungu kwa zawadi hii ya Roho Mtakatifu, bni vizuri ukifanya maombi haya kwa sauti na endapo unasikia ndani yako hali ya kutamka maneno usiyoyafahamu wakati huu basi endelea kutamka maneno hayo.
Kwa msaada zaidi unaweza kutuandikia comment hapo chini na ukaweka namba yako ya simu au whatasapp nasi tutakurudia na kuomba pamoja na wewe.