KANUNI YA MSINGI KATIKA KUNENA KWA LUGHA.

Kama vilivyo vipawa (zawadi) zote kutoka kwa Mungu kwenda kwa mwanadamu, kusudi kuu na la msingi la Kunena kwa Lugha ni kwa ajili ya kuujenga ufalme wake hapa duniani. Na Ufalme wa Mungu unawakilishwa hapa duniani na mwili wa Kristo, na huo mwili wa Kristo unaundwa na waamini wote waliomo duniani.Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri kabisa kwamba lengo la Kunena kwa lugha ni kuujenga mwili wa Kristo.

Na ili mwili ujengwe lazima kila kinachokusudiwa kuujenga huo mwili kifanyike katika upendo. Hivyo basi kanuni ha msingi ya kunena kwa lugha kama ilivyo kwa karama nyingine zozote ni kutenda katika upendo.

Sasa kabla hatujaingia ndani kuzungumzia kanuni hii ya msingi ya kunena kwa lugha yaani upendo, naomba uniruhusu nikuonyeshe kwa ufupi, namna gani kunena kwa lugha kunavyosaidia ujenzi wa mwili wa Kristo.

Kuna namna mbili kuu ambazo kunena kwa lugha kunasaidia ujenzi wa mwili wa Kristo.

1. Unakujenga wewe mwenyewe Mnenaji ambaye ni kiungo cha huo mwili.

2.Unalijenga Kanisa pale ambapo ujumbe uliokuja kwa lugha utayafasiriwa kwa ajili ya Kanisa.

Hebu tusome mistari hii katika kitabu cha  1Kor 14:1-5

“1 Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za Rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.

2 Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika Roho yake.

3 Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.

4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga Kanisa.

5 Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi Kanisa lipate kujengwa.”

Mada kuu katika maandiko hayo hapo juu ni kusisitiza kuhutubu kama jambo kuu zaidi kuliko kunena kwa lugha, kwa sababu kunena kunamjenga mnenaji na kuhutubu kunalijenga Kanisa. Lakini ukisoma maandiko hayo kwa makini utapata kujifunza sana kuhusu kunena kwa lugha na faida yake katika mwili wa Kristo. Sasa hebu tuangalie kwanza nini maandiko yanasema kuhusu kunena kwa lugha kabla hatujaangalia habari ya kuhutubu.

1.Maandiko yanatuonyesha kwamba  mtu akinena kwa lugha anajijenga nafsi yake.

2.Maandiko pia yanatuonyesha, kile kinachonena kikitafsiriwa, kinajenga Kanisa.

3.Kunena + Kufasiri ni sawa na kuhutubu.

Kwa maana hiyo kumbe nikinena kwa lugha ninajijenga nafsi yangu mwenyewe. Kwa hiyo kama kila anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake, basi Kanisa zima likinena kwa lugha maana yake kila mmoja atakuwa amejijenga nafsi yake na kuimarika zaidi. Na kama sisi ni viungo vya mwili wa Kristo ina maana kila kiungo kitakuwa kimeimarika na hivyo kufanya mwili wa Kristo kuimarika pia. Hii ni ‘dimension’ moja ya jinsi ambavyo kunena kunavyoweza kuujenga mwili wa Kristo. Changamoto ya ‘dimension’ hii ni kwamba sio wote katika mwili wa Kristo watakuwa na kiwango sawa cha kunena na hivyo basi sio wote katika mwili watakuwa na kiwango sawa cha kujengwa. Kwa mantiki hiyo ili kufikia usawa na uendelevu wa ujenzi wa mwili wa Kristo kunahitajika njia nyingine ambayo maandiko yanatuambia kuwa ni kuhutubu au kunena kwa lugha na kufasiri.

Kwa hiyo pale ambapo kile kilichonenwa kimetafsiriwa kwa lugha inayoeleweka na watumiaji. Kwa mfano tuseme hayo yaliyonenwa kwa lugha yametafsiriwa kwa Kiswahili katika Kanisa la watu wanaozungumza kiswahili, maana yake yatakuwa yamewajenga wale wote waliosikia na hivyo basi ni sawa na mtu anayehutubu katika Kanisa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inayoeleweka na hao wasikilizaji.

Sasa mambo yote hayo mawili ili yawe na faida kwa Kanisa lazima yanapaswa kujengwa katika upendo na sio katika mashindano au majivuno.

Unapofanya kazi katika vipawa vya Roho Mtakatifu nnje ya upendo unakuwa unafanya kinyume kabisa na lengo kuu la Mungu kuachilia vipawa vya Roho Mtakatifu.

Kwa hiyo hata siku moja usiingie kwenye mtego wa kunena kwa lugha eti kwa sababu unataka kujionyesha kuwa wewe unafanya vyema zaidi kuliko ndugu yako au kuonyesha ukomavu na ubora wako, au kujiimarisha na kuwa bora kuliko wengine. Kunena kwa lugha kunapaswa kuwa na faida ya kulijenga Kanisa (aidha kwa kuimarisha kiungo kimoja kimoja kwa lengo la kuimarisha wengine au kuimarisha viungo vyote kwa pamoja kwa njia ya kunena na kufasiri yale uliyoyapata sirini).

Sasa hebu tuangalie maandiko hayo hapo juu kwa upana wake kama yalivyo andikwa na Roho Mtakatifu kupitia kwa Paulo. Tunaona hapa Roho Mtakatifu analisisitiza Kanisa la Korintho kuhusu kuimarisha mwili wa Kristo kwa kuzingatia upendo. Na kwa kanuni hii ya msingi ya upendo, paulo akipima huduma hizi mbili kati ya kunena kwa lugha na kuhutubu anaona kuhutubu ni muhimu zaidi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa kuliko kunena kwa lugha.

Lakini katika mstari wa tano (5) anaonyesha pia kuwa kunena kwa lugha + kufasiri ni sawa na kuhutubu.

Inavyoonekana Kanisa hili la Korintho lilikuwa limezidisha (Overstretched) fundisho hili la kunena kwa lugha  katika kiwango ambacho inawezekana walikuwa wakitumia karama hii isivyopaswa.

Ukifuatilia vizuri Kanisa la Korintho linaonekana lilikuwa limesheheni karama za Roho Mtakatifu lakini lilikuwa   changa sana kiroho.Hii inaweza ikakushangaza kwamba Kanisa linawezaje kusheheni vipawa vya Roho Mtakatifu halafu likawa changa lakini ukweli ni kwamba ukomavu wa Kanisa au mtu haupimwi kwa utendaji wa karama za Roho (kwani karama ni zawadi na hutolewa bure ) bali ukomavu wa tabia katika kufikilia cheo cha utimilifu wa Kristo unakotokana na ushirikiano wako na Roho Mtakatifu katika kutii na kuenenda katika njia anayokuongoza.

Kwa hiyo Kanisa hili linaonekana lilipunguza matumizi ya kuhutubu na kuweka kunena palipokuwa panahitaji kuhutubu. Kwa hiyo kimsingi walikuwa hawajengani, bali kila aliyenena alijijenga mwenyewe na yule asiyenena aliachwa solemba bila kujua kinachoendelea wala kujua Mungu anasema nini. Na hapa ndio umuhimu wa kuwa na hekima na kuto ‘ku-overstrexh doctrine’ yeyote kwani unaweza ukajikuta unafanya unachokifanya pasipo kutimiza kusudi la awali la Mungu la kufanyika kwa hicho kinachofanyika.

Pasipo upendo hakuna ambaye anaweza kujitoa kwa ajili ya kuwajenga wengine na hatimaye kulijenga Kanisa. Kwanza ufahamu ya kwamba kitu chochote kinachokuletea faida wewe binafsi kinafurahisha na unaweza jikuta unaendelea kufurahia wewe mwenyewe pasipo kuwafaidisha wengine. Kwa hiyo hata katika kunena unaweza  kujikuta kila wakati unajijenga wewe mwenyewe  na ukasahau kabisa kufanya yale yanayoujenga mwili wa Kristo kama vile kuhutubu. (hapo mbele kidogo tutaangazia maana ya kuhutubu na hiyo itakusaidia kuona umuhimu wa kuhutubu katika mwili wa Kristo sambamba na kunena kwa lugha)

Biblia inasema ahutubuye anaongea na watu, bali anenaye anaongea na Mungu. anenaye anajijenga yeye mwenyewe bali ahutubuye analijenga Kanisa. ukinena na kufasiri ulichonena unakuwa sawa na anayehutubu kwani zile siri za rohoni unaziwasilisha kwa Kanisa zima na hivyo mwili mzima unajengwa.

Ukinena pasipo kufasiri unajijenga wewe mwenyewe, unajifariji wewe mwenyewe na kujitia moyo wewe mwenyewe.

Kwa hiyo usipokuwa na upendo unaweza ukajikuta unajijenga wewe mwenyewe pasipo kujali maendeleo ya mwili wa Kristo ukoje, na ukakuwa wewe mwenyewe wakati mwili wa Kristo unapata shida. Hivyo ni lazima sana ku ‘strike a balance’ kati ya kunena na kuhutubu, na kujuwa ni wakati gani wa kunena na wakati gani wa kuhutubu ili mwili wa Kristo ujengwe. Biblia pia anatupa angalizo katika 1Kor 2 :1-2

“1 Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo  na upatu uvumao.

2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. ‘

Mbona haya mambo paulo anayoyasema ndio wengi katika mwili wa Kristo wanayatamani?, inakuwaje paulo anasema ukiwa na hayo yote lakini hauna upendo si kitu, tena ni sawa na shaba iliayo na upatu uvumao, ni kwa sababu pasipo upendo hayo yote hayawezi kuufaidia mwili wa Kristo, na Mungu ametuweka hapa duniani katika mwili wake ili tufaidiane. hebu soma tena Waefeso 4:11-13

“11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Unaona hapo, kusudi la Mungu kuachilia karama, huduma, vipawa na neema zake zote ni ili mwili wake ujengwe na chochote hata kama kinaonekana ni kizuri kiasi gani kikiwa kinyume na kusudi hilo kinakuwa ni chukizo kama ilivyokuwa kwa kusudio la kujenga mnara wa babeli. kwa hiyo ndugu ukitaka kukua na kufaidi kunena kwa lugha lazima nia yako kuu iwe katika upendo na hapa upendo unaona ni kuwa wa utumishi na kulenga kuujenga mwili wa Kristo na sio kujijenga wewe mwenyewe tu kwa tamaa binafsi (selfish desires).

Kwa hiyo basi wanaofaidika na watakaofaidika sana na kunena kwa lugha ni wale ambao lengo lao na kusudi lao ni kuujenga mwili wa Kristo, kwani Mungu anaaangalia nia ya ndani ya kila mmoja tofauti na sisi wanadamu tunaoangalia sura na muonekano wa nnje.

Mungu akubariki sana.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *