Tulipokuwa tunaangazia maana ya kunena kwa lugha tulihitimisha kwa kusema kuwa Kunena kwa lugha ni uwezo wa lugha ya kiungu wa kufanikisha mambo mengi kwa sababu nyingi za kiroho.
Mambo yafuatayo ni sehemu ya mambo makuu ambayo kunena kwa lugha kunayafanikisha kwa sababu kadha wa kadha za kiroho;
- Kunena kwa lugha kama ishara,
- Kunena kwa lugha kama Ushahidi wa kujazwa Roho Mtakatifu,
- Kunena kwa Lugha kama ibada, na;
- Kunena kwa lugha kama Karama.
Ukifuatilia Habari ya kunena kwa lugha kibiblia utaona kuwa kunena kwa lugha kunafanikisha mambo haya makubwa manne na katika sura hii tutaangazia kwa undani kila jambo tajwa hapo juu.
Ninaweza kusema kuwa hapa ndipo siri kubwa ya kunena kwa lugha ilipojificha na mtu usipokuwa makini unaweza kujikuta ukichanganya haya mambo na hatimaye ukadogosha umuhimu wa kunena kwa lugha au kuukanusha kabisa na hatimaye kukosa faida nnzuri zilizokusudiwa na Mungu katika kunena kwa Lugha.Hebu tuanze na jambo la kwanza.
KUNENA KWA LUGHA KAMA ISHARA
Hapo mwanzoni tumeona orodha ya ishara aliyoitoa Yesu ya kumtambua mtu ambaye ni muamini sawasawa na kitabu cha Marko 16:17- 18 kuwa ni;
- Kutoa pepo Kwa jina ka Yesu.
- Kusema kwa Lugha Mpya
- Kushika nyoka
- Kutokudhuriwa kabisa hata wakinywa kitu cha kufisha.
- Kuweka mikono yao juu ya wagonjwa na wagonjwa kupata afya.
Kwa maneno ya Yesu mwenyewe anasema;
“17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Katika kitabu cha Mdo 1: 8 biblia inasema:
“8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
Tukisoma maandiko haya mawili kwa pamoja, utagundua kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ujazo wa Roho Mtakatifu + Nguvu + Ishara + kuwa shahidi wa Yesu.
Sasa hapa kuna jambo ambalo linadhihirika siku ambayo wanafunzi wanajazwa Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza, sawasawa na Mdo 2
Tunaona katika maandiko haya baada ya Roho Mtakatifu kuwajilia wanafunzi juu yao wanaanza kusema kwa lugha mpya kama roho alivyowajalia, na punde tunaona wanapata ujasiri wa kulisema Neno kwa wale wasioamini na wanapata mavuno ya roho elfu tatu zinazoamini na kumkiri Yesu.
Tunaona
- Ndimi kama za moto ziliwakilisha Roho Mtakatifu.
- Kunena kwa lugha kulikuwa ishara.
- Ujasiri wa kusimama kwenye lile kundi na kuhubiri kulionyesha kuwa wamekuwa mashahidi imara wa Yesu.
- Na ule ujasiri na matokeo waliyoyapata yanadhihirisha kulikuwa na nguvu ndani yao.
Kwa hiyo hapo tunaona ishara ya kunena kwa lugha inajitokeza baada ya wanafunzi kujazwa Roho Mtakatifu.
Kwa hiyo ishara ya kunena kwa lugha inadhihirika hapa na inadhihirika kwa wanafunzi kunena kwa lugha za kibinadamu zilizokuwa zikizungumzwa kwa jamii ya wayahudi toka mataifa mbalimbali yenye lugha tofauti tofauti.
Sasa pale ambapo kunena kwa lugha ni ishara kwa wasio waamini kuwa mnenaji ni muamini mara nyingi yafuatayo yanatokea,
- Lugha inayozungumzwa inakuwa ya wanadamu na wasikilizaji wanaifahamu japo kuwa mnenaji hana ufahamu wala ujuzi kwayo.
- Mnenaji ananena matendo makuu ya Mungu ambayo yanagusa mioyo ya wanaosikia na wanashindwa kuelewa mnenaji amejuaje kama sio Mungu amemfunulia.
- Ishara hiyo inawapelekea wale wanaosikia kumuamini Yesu na kumpokea kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yao.
Maandiko katika kitabu cha mdo 2:11-12 ni mfano thabiti wa hoja hii
“…tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?”
Kumbuka mshangao huu ulitokea kwa sababu wale waliokuwa wakisema hayo matendo makuu walikuwa wakiyasema kwa lugha za wasikilizaji, lugha ambazo wanenaji hawajajifunza wala walikuwa hawawezi kuziongea hapo awali isipokuwa bada ya kupokea uwezo kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Kitabu cha isaya 28:11, ni moja ya maandiko machache katika agano la kale ambalo linazungumzia kunena kwa lugha na kimahususi kabisa kuhusu kunena kwa lugha kama ishara.Mstari huu unasema;
“11. Haya basi! Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa kwa njia ya watu wa lugha tofauti wanaoongea lugha ngeni.
Andiko hili pia linanukuliwa katika kitabu cha 1 Kor 14:21-22 (a).
“21 Imeandikwa katika torati, Nitasema na watu hawa kwa watu wa lugha nyingine, na kwa midomo ya wageni, wala hata hivyo hawatanisikia, asema Bwana.
22 Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini…” Mpaka hapa tulipofika tunaona “dimension” moja wapo ya kunena kwa lugha kuwa ni ishara kwao wasioamini. Tutaendelea tena kuangalia dimensions nyingine kwani Ushahidi wa maandiko unaonyesha kuwa kunena kwa lugha hakuishii katika ishara peke yake..