Kitabu cha matendo ya mitume ndio kitabu kilichohifadhi kwa kina kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu kuanzia kwa mitume, Kanisa la Samaria,Kornelio na familia yake, Mtume Paulo na Kanisa la Efeso.
Wasomi wa Historia wa kanisa wanasema kipindi cha kuanzia siku ya pentekoste mpaka kanisa la efeso linajazwa na Roho Mtakatifu ni kipindi cha zaidi ya miaka ishirini. Kwa hiyo tunapozungumzia matukio Matano ya ujazo wa Roho Mtakatifu yaliyorekodiwa katika kitabu cha matendo ya mitume tunazungumzia matukio Matano yaliyotokea ndani ya miaka ishirini.
Kwa hiyo unaweza kukubaliana nami kwamba lazima matukio ya kujazwa Roho Mtakatifu kwa waamini yalikuwa ni mengi zaidi ya yale ambayo yamerekodiwa lakini kwa hekima za Mungu na kwa muktadha wa kitabu cha Matendo ya mitume matukio haya Matano yanatosha kutonyesha “parten” ya kujazwa Roho Mtakatifu.
Sasa naomba tuangalie maandiko yanayoonyesha matukio hayo hapo juu, halafu baada ya hapo tutayachambua kuona “parten” ya ujazo wa Roho Mtakatifu ulivyoonyeshwa katika maandiko.
Ujazo wa Roho Mtakatifu kwa wanafunzi Mia na Ishirini (120) wa kwanza
Mdo 2:4
” Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”
Ujazo wa Roho Mtakatifu kwa Kornelio na familia yake.
Mdo 10:44-46
” 44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,”
Ujazo wa Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Efeso.
Mdo 19:6
“Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”
Katika maeneo yote matatu hapo juu, tunaona ushahidi wa moja kwa moja wa kimaandiko ukionyesha kuwa punde tu baada ya watu hawa wote kujazwa Roho Mtakatifu walianza kunena kwa lugha mpya.
Kwa ushahidi huu wa moja kwa moja tuko sahihi kabisa kusema kwamba kunena kwa lugha ni ushahidi wa awali wa mtu kujazwa Roho Mtakatifu.
Hapo juu tulisema kuwa katika kitabu cha matendo ya mitume kuna sehemu tano zilizoonesha watu wakijazwa Roho Mtakatifu na kati ya hizo tano kuna ushahidi wa moja Kwa moja wa kimaandiko unaoonyesha kuwa watu wale punde tu baada ya kujazwa roho mtakatifu walianza kisema kwa lugha mpya. Lakini ukiangalia sehemu zile mbili zilizobaki utaona kuna ushahidi wa kimazingira unaoonyesha kuwa watu wale pia walinena kwa lugha. Hebu sasa tuangazie mifano hiyo miwili.
Mifano hii miwili ni mfano wa Kanisa la Samaria baada ya Petro na Yohana kwenda na kuwaombea watu wale ujazo wa Roho Mtakatifu na mfano wa pili ni Paulo baada ya kuombewa na Anania.
Hebu tusome maandiko;
Mdo 8:14-20
14. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;
15. ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;
16. kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.
17. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.
18. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,
19. Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu
20. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.
Ukiangalia Kanisa la Samaria, Biblia haisemi wazi wazi kuwa watu hawa walinena kwa lugha punde baada ya kujazwa Roho Mtakatifu, lakini swali ambalo ninataka tujiulize ni je ni kitu gani ambacho huyu ndugu Simoni, aliona ambacho kilimshawishi kuwa watu hawa wamempokea Roho Mtakatifu mpaka akawa radhi kutaka kulipia uwezo huo na kipawa hicho cha kuwekea watu mikono ili wapokee Roho Mtakatifu?
Ushahidi wa kimazingira na mtiririko wa matukio yale matatu yaliyopita,unashawishi kuwa alichokiona Simoni ni kitendo cha kunena kwa lugha punde baada ya watu wale kuwekewa mikono na kupokea Roho Mtakatifu.
Kwa habari ya Paulo kitabu cha Matendo ya Mitume Sura ya 9:17-22 inaeleza habari za Paulo kujazwa Roho Mtakatifu.
17. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;19. Akala chakula,na kupata nguvu.
20. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?
22. Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
Katika maandiko haya, hatuoni pia ushahidi wa moja kwa moja wa Paulo kunena kwa lugha baada ya kujazwa Roho Mtakatifu, lakini tukisoma kitabu cha 1 Wakorintho 14:18 tunaona Paulo akikiri na kusema;
“Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote;”
Kwa hiyo kwa andiko hili la Wakorintho, tunapata uthibitisho toka kwa Paulo mwenyewe kuwa ananena kwa lugha, na anaujasiri wa kuwaambia kanisa la Wakorintho kuwa ananena kwa lugha zaidi yao wote. Kwa hiyo kwa muktadha wa somo letu swali hapa sio kama Paulo ana nena kwa lugha ama la, bali swali letu hapa ni je Paulo alianza lini kunena kwa Lugha? Swali hili halina jibu la moja kwa moja lakini kama tulivyoona hapo juu kati ya mifano mitano, minne tunaona watu wakinena kwa lugha baada ya kupokea Roho Mtakatifu basi tutakuwa salama tukisema hata Paulo naye alinena kwa lugha baada ya kujazwa Roho Mtakatifu.
Hitimisho hili pia linapewa nguvu na uzoefu katika huduma ya ujazo wa Roho Mtakatifu ambao unaonyesha Ushahidi huu wa kunena kwa lugha ukiambatana na ujazo wa Roho Mtakatifu.
Amina