A. Maana na lengo la ibada.
” Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.
Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”(Mathayo 4:5)
Ibada ni kitendo cha mwanadamu kumsujudia na Kumuabudu Mungu wa kweli wa pekee na hai.
Lengo la ibada ni kusifu, kusujudu , kumuadhimisha na kuonyesha utegemezi wako kwa Mungu na mamlaka yake ambayo unakubali kuwa iko juu kuliko wewe unayefanya ibada.
Mwanadamu kwa utashi wake anaweza kutumia nafasi yake kuabudu kitu kingine kuacha Mungu wa kweli, lakini ukifanya hivyo unakuwa umefanya ibada ya sanamu na hiyo inakuwa sio ibada ya kweli.
Wanadamu inatupasa kumsujudia Bwana Mungu, na kumuabudu yeye peke yake. Kuabudu kitu kingine chochote ni chukizo mbele za Mungu.
Katika Biblia tunaona ibada kuanzia mwanzo kabisa wa uwepo wa mwanadamu. Katika kitabu cha Mwanzo 3:8-11 unaona Sauti ya Mungu ikija Bustanini na Adam na eva wanajificha, hii inaonesha kuwa kabla ya tukio la kula tunda kulikuwa na fellowship kati ya Mungu na Adam na mkewe.
Lakini pia baada ya anguko tunawaona Kaini na Habili wakitoa sadaka zao kwa Mungu, haya yote ni viashiria vya uwepo wa ibada. Tukio hili linakwenda mbele zaidi kwa Kaini kumuua ndugu yake Habili baada ya sadaka yake kukubalika na ya kaini kukataliwa. hii inaweza kuwa picha ya ibada iliyo sahihi na ibada ambayo haikuwa sahihi.
Mwanzo 4:25-26, inarekodi habari inayotupa mwanga mwingine kuhusu ibada, Biblia inasema;
“25 Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana”
Maandiko haya yanaonyesha hapa ndipo ulikuwa mwanzo wa watu kuliitia jina la Bwana, kumtegemea Mungu na kumshirikisha Mungu katika masuala yao. Tunaona wazi kabisa biblia ikieleza kwamba “…Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.
Kwa hiyo kwa tafsiri ya maandiko haya, kabla ya hapo watu walikuwa hawaliitii jina la Bwana, au unaweza kusema hakukuwa na mfumo thabiti wa watu kufanya utegemezi wao kwa Mungu. au Mwanadamu hakutambua katika maisha yake ya kila siku kuwa anauhitaji wa kuliitia jina la Mungu mpaka kipindi hiki ambacho Sethi alimzaa Enoshi. Kwa lugha nyingine Sethi anakuwa ni chimbuko la watu kumtambua Mungu na kumfanyia Ibada.
Mtiririko huu wa ibada unaendelea mbele zaidi ambapo Henoko naye anatajwa kutembea na Bwana(Mwanzo 5:24), na Nuhu anatajwa kusikia na kutii sauti ya Bwana (Mwanzo 6:9).
Kutoka kuliitia jina la Bwana kwa seth, tunaona mtu katika kizazi cha sita (Henoko) anatembea na Bwana na katika kizazi cha tisa (Nuhu) mahusiano ya kiibada kati ya Mungu na mwanadamu yanaimarika zaidi. Hii haimaanishi kwamba wanadamu katika dunia yote waliimarisha mahusiano, la hasha lakini palikuwa na mtu aliyeweza kuimarisha mahusiano.
Vizazi vingi baada ya nuhu zaidi ya 15 anatokea mtu mwingine ambaye anaonesha uhusiano mzuri wa kiibada na Mungu, mtu huyu si mwingine bali ni ibrahimu na Mungu anamuahidi uzao wake kuwa mzao mteule, hatimaye isaka na halafu yakobo.
Hatuna muda wa kueleza kwa kina mtiririrko wa matukio ya kihistoria kuhusu ibada lakini tunajifunza kuanzia seth mpaka wana wa Israel ibada ilihusisha mambo kadha wa kadha yakiwamo;
- Unyenyekevu wa moyo
- Maombi
- Imani
- Utegemezi kwa Mungu
- Shukrani
- Sadaka/ dhabihu
- Madhabahu
- Utii wa maelekezo ya Mungu.