Kunena kwa lugha ni uwezo wa mtu anayemuamini Yesu (aliyeokoka) kuzungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, lugha (inayoeleweka kibinadamu au isiyoeleweka kibinadamu) ambayo kwa akili za kawaida mtu huyo haifahamu wala hajawahi kujifunza lugha hiyo.
Kwa maana hiyo hapo juu tunaona vipengele vikuu vitatu vya kunena kwa lugha ambavyo ni;
1. Kunena kwa lugha kunatendwa na Mtu anayemuamini Yesu (Aliyeokoka).
Kunena kwa lugha ni uwezo maalumu wa kiMungu kwa waamini (watu waliokoka). Mtu ambaye si muamini (hajaokoka) hawezi kunena kwa lugha wala kuwa na uwezo wa kunena kwa lugha kwani, kunena kwa lugha ni moja ya ishara za watu wanaomuamini Yesu.
Yesu mwenyewe katika kitabu cha Marko 16:17-18 anasema
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Hivyo basi anayenena kwa lugha ni lazima awe muamini na si vinginevyo.
Kama wewe bado hujaokoka na unataka kufaidi zawadi hii ya Mungu kwa wanadamu, unaweza kuifaidi kwanza kwa kuokoka ambapo biblia katika kitabu cha Warumi 10:9-10 inasema;
” Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”
Hivyo basi kama unaamini kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu na uko tayari kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu ni Bwana sema sala hii kwa sauti na utakuwa umeokoka na utafaidi yote yanayosemwa katika kitabu hiki kwa maana ya Kunena kwa Lugha na faida ziambatanazo na Kunena kwa Lugha. Sema maneno haya kwa sauti;
“Eee Bwana Yesu, ninatubu dhambi zangu, karibu moyoni mwangu, uwe Bwana na Mwokozi wa Maisha yangu. Amen”.
Hongera sana kwa kusema sala hii, kama umesema ukiwa unaamini kuwa Mungu alimfufua Yesu katika wafu,basi wewe umekwisha okoka.
2. Kunena kwa Lugha kunafanyika kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Anayenena kwa lugha ni mwanadamu aliyeokoka, lakini kunena huko hakufanyiki kwa uwezo wa kibinadamu bali kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Kwa maneno mengine, uwezo wa kunena kwa lugha haufanyiki kwa mafunzo, mazoezi au kujizoeza, uwezo wa kunena kwa lugha ni uwezo wa Roho Mtakatifu ndani ya muamini. yaani anayezungumza ni mtu, lakini uwezo wa kuweza kuzungumza hayo anayoyazungumza unatoka kwa Roho Mtakatifu.
Kumbuka, mafunzo, mazoezi na kujizoeza hakuleti uwezo wa kunena kwa lugha bali kunaweza kuongeza ufanisi. UWEZO WA KUNENA NA MANENO GANI YA KUTAMKA ni mamlaka ya kipekee (exclusive jurisdiction) ya Roho Mtakatifu pekee.
Hebu tuangalie mara ya kwanza waamini kunena kwa lugha ilikuwaje;
“Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Mdo 2:4
Tunaona baada ya kujazwa Roho Mtakatifu, wanafunzi walianza kusema kwa lugha nyingine, KAMA ROHO ALIVYOWAJALIA KUTAMKA”
Kwa hiyo wakati wowote unaponena kwa lugha hakikisha unategemea uwezo wa Roho Mtakatifu na sio uwezo wako mwenyewe. Kadiri tunavyoendelea tutajifunza zaidi hili linatokeaje.
a) Lugha inayozungumzwa yaweza kuwa lugha inayozungumzwa hapa duniani.
Tumeona hapo juu kuwa kunena kwa Lugha kunatendwa na Mtu anayemuamini Yesu na kunatendwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kwamba maneno yanayotamkwa ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
La muhimu kujifunza hapa ni kwamba kati ya maneno ambayo Roho Mtakatifu atakuwezesha kutamka yanaweza kuwa maneno ya lugha zinazozungumzwa na wanadamu au lugha ambazo hazifahamiki kabisa katika jamii za wanadamu. Kadiri tunavyoendelea kujifunza utaona kuwa lugha inayozungumzwa ikiwa ni ha kibinadamu, malengo yake yanakuwa tofauti na pale ambapo lugha inayozungumzwa sio ya kibinadamu.
Tunaona katika Mdo 2:5-12
” 5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.
6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia,
10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?”
Tunaona hapa lugha ambazo waamini walizisema kwa uwezo wa Roho Mtakatifu baada ya kupokea Roho Mtakatifu ilikuwa ni lugha ambazo zilikuwa zikizungumzwa na wanadamu katika jamii tofauti takribani kumi na saba.
Kitendo cha jamii hizi kushangaa na kuingiwa na hofu kwa wagalilaya hawa kuzungumza lugha zao kunaonyesha kulikuwa na ufasaha wa hali ya juu wa lugha, maneno, matamshi na lafudhi katika kuzungumza kwao kwa namna ambayo wengi waliosikia matendo makuu ya Mungu aliyotamka kwa kinywa cha wale wanafunzi kwa lugha za wale wasikilizaji.
b) Lugha inayozungumzwa yaweza kuwa lugha isiyoeleweka na mwanadamu yeyote hapa duniani.
Biblia sehemu Nyingine inaonyesha kuwa kunena kwa lugha kunaweza kuwa kwa lugha isiyoeleweka na mwanadamu yeyote. Katika kitabu cha 1Kor 14:2 biblia inasema;
“Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”
Mstari huu unaonyesha aina ha kunena ambayo si kwa lugha ambazo zinasikika au kueleweka na wanadamu, ambako katikati ya jamii ya waamini ndio inayojulikana zaidi kuliko aina ile ya kunena lugha inayofahamika na wanadamu.
Kitabu cha 1Kor 13(a) kinatupa pia dodoso ya aina hii ya kugha pale mwandishi anaposema;
“Nijaposema Kwa lugha za wanadamu na za malaika,”
Kwa hiyo lugha zinazoeleweka tunaweza pia kuziita lugha za wanadamu na zile zisizoeleweka kibinadamu tunaweza kuziita lugha za malaika.kwa hiyo kwa sababu hakuna mwanadamu anayeelewa kugha hiyo unayonena usije ukadhani sio lugha, hiyo ni lugha ya malaika, unayozungumza nayo na Mungu na ambayo unaizungumza kutoka rohoni, roho iliyozaliwa upya kwa kumuamini na kumkiri Yesu Kristo.
Jambo la msingi kukumbuka ni kwamba aina yeyote ya lugha inayozungumzwa aidha ni ya kibinadamu au sio, uwezo wa kuzungumza lugha hiyo lazima uwe ni uwezo wa Roho Mtakatifu na si vinginevyo.
3. Mtendaji hapaswi kuwa na ufahamu wala ujuzi wa lugha hiyo.
Kama unazungumza lugha ambayo unaufahamu au ujuzi katika hiyo basi huko sio kunena kwa lugha kunakozungumzwa na biblia. Kunena kwa lugha kunakozungumzwa na biblia ni uwezo wa kiungu ndani ya mwanadamu na unapotokea, akili za mzungumzaji haihusiki kabisa wala haina matunda. “There is no and there should be no natural comprehension by the speaker of the tongue.”
Biblia inasema
“Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.”1Kor 14:14
Sio tu kwamba unaponena akili zako hazitakiwi kuwa na matunda na ufahamu, lakini pia mtu anenaye hapaswi kuwa na uzoefu wa lugha husika.
Ufahamu wa unachokinena huja pale tu ambapo Mungu ataachilia uwezo mwingine wa kiungu ndani yako wa kufasiri Lugha na si vinginevyo.
Kunena wa lugha ni uwezo wa lugha ya kiungu kufanikisha mambo mengi kwa sababu nyingi za kiroho.
Mungu akubariki sana, unaweza kusoma utangulizi wa somo hili hapa.
Pingback: SIRI YA KUNENA KWA LUGHA:UTANGULIZI. – King's Life School